Mabomu yarindima Dar:Ni wakati polisi wakizuia maandamano ya CUF
Dar es Salaam. Polisi jijini Dar es Salaam jana walifyatua mabomu ya
machozi kutawanya viongozi na wafuasi wa CUF na baadaye kumtia nguvuni
Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 32, tukio lililosababisha Ukawa
kuunganisha nguvu kuwasaidia kuandika maelezo.

Mwenyekiti wa CUF Profesa Ibrahim Lipumba,
akiwa chini ya ulinzi wa Polisi Dar es Salaam jana, baada ya kukamatwa
kwa yeye na wafusi 36 wa Chama hicho 32 madai ya kuandamana bila
kibali cha polisi, kukumbuka mauaji ya wafuasi 22 wa Chama hicho huko
Pemba, Januari 26 na 27 , 2001 baada ya polisi kupambana na
waandamanaji. Picha na Saidi Khamis.
Profesa Lipumba na viongozi wenzake walikuwa wakienda Zakhem, Mbagala
kuwatawanya kwa amani wafuasi wa CUF baada ya Jeshi la Polisi kutoa
taarifa mapema jana ya kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara
uliopangwa kwa ajili ya kuadhimisha miaka 14 tangu wafuasi wa chama
hicho walipouawa kwa risasi na polisi wakati wakiandamana kupinga
matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2001. Maandamano hayo
yalipangwa kuanzia Temeke Mwisho na kuishia Mbagala Zakhem wilayani
Temeke ambako chama hicho kina nguvu kubwa.
Lakini azima yao ilikumbana na mkono wa dola baada ya polisi kuwazuia
viongozi hao eneo la Mtoni Mtongani na baadaye kutumia nguvu kutawanya
wananchi.
Katika sakata hilo, polisi waliwaweka chini ya ulinzi viongozi wote
akiwamo Profesa Lipumba na wafuasi hao walipokuwa wakijiandaa kwenda
Viwanja vya Zakhem, ambako mkutano ungefanyika.
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilithibitisha kukamatwa kwa
Lipumba na wanachama 32 wa CUF kwa kufanya maandamano haramu na walikuwa
Kituo Kikuu cha Polisi, ambako viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) walienda pamoja na wanasheria waliotakiwa kuwasaidia kuandika
maelezo.
No comments:
Post a Comment